Surah An-Naml (The Ants)

Listen

Swahili

Surah An-Naml (The Ants) - Aya count 93

طسۤۚ تِلۡكَ ءَایَـٰتُ ٱلۡقُرۡءَانِ وَكِتَابࣲ مُّبِینٍ ﴿١﴾

T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu kinacho bainisha; .

T'aa Siin, (T' na S) harufi mbili za kutamkwa, ni harufi za alifbete, ndizo zimeanzia Sura hii, ili kunabihisha siri ya muujiza wa Qur'ani pamoja na kuashiria kuwa imeundwa kwa jinsi ya harufi hizi hizi mnazo zitumia katika kusema, na pia kuzindua akili ziisikilize hii Qur'ani inapo somwa. Hizi Aya zilizo teremka kwa kusomwa, na ni Kitabu chenye kubainisha mambo yaliyo kuja ndani yake.


Arabic explanations of the Qur’an:

هُدࣰى وَبُشۡرَىٰ لِلۡمُؤۡمِنِینَ ﴿٢﴾

Uwongofu na bishara kwa Waumini!

Na hii Qur'ani ni Uwongofu wa kuwaahidi Waumini waifuate njia ya kheri, na kufuzu duniani na Akhera, na inawabashiria kuwa watapata malipo mazuri.


Arabic explanations of the Qur’an:

ٱلَّذِینَ یُقِیمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَیُؤۡتُونَ ٱلزَّكَوٰةَ وَهُم بِٱلۡـَٔاخِرَةِ هُمۡ یُوقِنُونَ ﴿٣﴾

Ambao wanashika Swala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo.

Waumini hao ndio wanao ishika Swala kwa unyenyekevu na kutimiliza nguzo, na wanatoa Zaka kwa nyakati zake, nao wana yakini ya maisha ya baadaye Akhera, na yatayo kuwa huko ya adhabu na thawabu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّ ٱلَّذِینَ لَا یُؤۡمِنُونَ بِٱلۡـَٔاخِرَةِ زَیَّنَّا لَهُمۡ أَعۡمَـٰلَهُمۡ فَهُمۡ یَعۡمَهُونَ ﴿٤﴾

Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo.

Hakika wale ambao hawaiamini Akhera, Sisi tumewapambia vitendo vyao kwa kuwaumbia matamanio ndani yake. Kwa hivyo wao wanababaika humo katika upotovu wao.


Arabic explanations of the Qur’an:

أُوْلَـٰۤىِٕكَ ٱلَّذِینَ لَهُمۡ سُوۤءُ ٱلۡعَذَابِ وَهُمۡ فِی ٱلۡـَٔاخِرَةِ هُمُ ٱلۡأَخۡسَرُونَ ﴿٥﴾

Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika Akhera ndio watapata khasara zaidi.

Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na Akhera ndio watakuwa khasarani kushinda wote.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنَّكَ لَتُلَقَّى ٱلۡقُرۡءَانَ مِن لَّدُنۡ حَكِیمٍ عَلِیمٍ ﴿٦﴾

Na hakika wewe unafundishwa Qur'ani inayo tokana kwake Mwenye hikima Mwenye kujua.

Ewe Nabii! Wewe unapokea Qur'ani hii unayo teremshiwa kutokana na Yeye ambaye hapana anaye mkaribia kwa hikima yake, naye anajua kila kitu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِذۡ قَالَ مُوسَىٰ لِأَهۡلِهِۦۤ إِنِّیۤ ءَانَسۡتُ نَارࣰا سَـَٔاتِیكُم مِّنۡهَا بِخَبَرٍ أَوۡ ءَاتِیكُم بِشِهَابࣲ قَبَسࣲ لَّعَلَّكُمۡ تَصۡطَلُونَ ﴿٧﴾

(Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili mpate kuota moto.

Kumbuka pale Musa alipo mwambia mkewe na walio pamoja naye na yeye ndio anarejea Misri: Mimi nimeona moto. Nitakwenda kuleteeni khabari ya njia, au nitapata kijinga cha moto, kitacho kufaeni kwa kuota moto kwa hii baridi.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَلَمَّا جَاۤءَهَا نُودِیَ أَنۢ بُورِكَ مَن فِی ٱلنَّارِ وَمَنۡ حَوۡلَهَا وَسُبۡحَـٰنَ ٱللَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِینَ ﴿٨﴾

Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Alipo fika huko paliitwa: Wamebarikiwa waliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake, yaani karibu yake. Nao ni Malaika na Musa. Na Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote ametakasika na kila kisicho kuwa laiki naye.


Arabic explanations of the Qur’an:

یَـٰمُوسَىٰۤ إِنَّهُۥۤ أَنَا ٱللَّهُ ٱلۡعَزِیزُ ٱلۡحَكِیمُ ﴿٩﴾

Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kuweka kila kitu pahala pake.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَأَلۡقِ عَصَاكَۚ فَلَمَّا رَءَاهَا تَهۡتَزُّ كَأَنَّهَا جَاۤنࣱّ وَلَّىٰ مُدۡبِرࣰا وَلَمۡ یُعَقِّبۡۚ یَـٰمُوسَىٰ لَا تَخَفۡ إِنِّی لَا یَخَافُ لَدَیَّ ٱلۡمُرۡسَلُونَ ﴿١٠﴾

Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu Mitume.

Na katika njia ya kufikisha wito wako, tupa fimbo yako na utaiona inatikisika kama kijoka jepesi kinakwenda mbio. Yeye akarudi nyuma, wala hakurejea baada ya kurudi nyuma. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtuza kwa kauli yake: Usiogope. Mbele yangu hawaogopi. Mitume ninapo sema nao. Kisa cha Musa kimetajwa zaidi ya mara moja katika Qur'ani. Pengine hutolewa yasiyo tajwa penginepo. Na kila sehemu ina mnasaba wake. Katika sehemu hii makusudio ni kuondoa yale mastaajabu ya kuwa Nabii Muhammad s.a.w. kapata Ufunuoa (Wahyi) vile vile.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِلَّا مَن ظَلَمَ ثُمَّ بَدَّلَ حُسۡنَۢا بَعۡدَ سُوۤءࣲ فَإِنِّی غَفُورࣱ رَّحِیمࣱ ﴿١١﴾

Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.

Lakini mwenye kutenda asicho ruhusiwa, na kisha akaleta wema baada ya kuteleza kwake, basi Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mkubwa wa kurehemu.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَأَدۡخِلۡ یَدَكَ فِی جَیۡبِكَ تَخۡرُجۡ بَیۡضَاۤءَ مِنۡ غَیۡرِ سُوۤءࣲۖ فِی تِسۡعِ ءَایَـٰتٍ إِلَىٰ فِرۡعَوۡنَ وَقَوۡمِهِۦۤۚ إِنَّهُمۡ كَانُواْ قَوۡمࣰا فَـٰسِقِینَ ﴿١٢﴾

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe bila ya maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu waovu.

Na utie mkono wako katika mfuko wa nguo zako, utatoka mweupe wala si kwa balanga. Hayo ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu, ni makafiri. Hizo Ishara tisa ni:- Kupasuka bahari, T'ufani (Kimbunga), Nzige, Chawa, Vyura, Damu, Ukame, Fimbo, Kutoka mkono mweupe bila ya maradhi.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَلَمَّا جَاۤءَتۡهُمۡ ءَایَـٰتُنَا مُبۡصِرَةࣰ قَالُواْ هَـٰذَا سِحۡرࣱ مُّبِینࣱ ﴿١٣﴾

Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri.

Ilipo kuja miujiza hii kwa uwazi na dhaahiri wakasema: Huu ni uchawi wazi!


Arabic explanations of the Qur’an:

وَجَحَدُواْ بِهَا وَٱسۡتَیۡقَنَتۡهَاۤ أَنفُسُهُمۡ ظُلۡمࣰا وَعُلُوࣰّاۚ فَٱنظُرۡ كَیۡفَ كَانَ عَـٰقِبَةُ ٱلۡمُفۡسِدِینَ ﴿١٤﴾

Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!

Wakaikadhibisha miujiza wakikataa kuwa inaonyesha dalili ya Utume. Na hakika yakini ilikwisha waingia katika nyoyo zao, lakini hawakusalimu amri kwa kuwa walikwisha tangaza kufuata upotovu na kushika uasi. Basi ewe Nabii! Hebu angalia vipi yalikuwa matokeo ya walio shikilia ufisadi, wakaikanya miujiza nayo iko wazi.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَلَقَدۡ ءَاتَیۡنَا دَاوُۥدَ وَسُلَیۡمَـٰنَ عِلۡمࣰاۖ وَقَالَا ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ ٱلَّذِی فَضَّلَنَا عَلَىٰ كَثِیرࣲ مِّنۡ عِبَادِهِ ٱلۡمُؤۡمِنِینَ ﴿١٥﴾

Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye tufadhilisha kuliko wengi katika waja wake Waumini.

Hizo ndizo jeuri za Firauni kwa sababu ya ufalme wake. Hebu sasa angalia utawala muadilifu, utawala wa hukumu, utawala wa unabii wa Daudi na mwanawe, Sulaiman, Mwenyezi Mungu awape amani. Sisi tuliwapa ilimu nyingi za sharia na mazoezi ya kuhukumu. Wakasimamisha uadilifu, na wakamhimidi Mwenyezi Mungu aliye wapa fadhila kushinda wengi katika waja wake wenye kusadiki, na kuifuata Haki.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَوَرِثَ سُلَیۡمَـٰنُ دَاوُۥدَۖ وَقَالَ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلنَّاسُ عُلِّمۡنَا مَنطِقَ ٱلطَّیۡرِ وَأُوتِینَا مِن كُلِّ شَیۡءٍۖ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ ٱلۡفَضۡلُ ٱلۡمُبِینُ ﴿١٦﴾

Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri.

Ufalme na hukumu ukatoka kwa Daudi ukenda kwa mwanawe, Sulaiman; naye akasema: Enyi watu! Sisi tumefunzwa lugha ya ndege, na tumepewa mengi tunayo yahitajia katika utawala wetu. Hakika neema hizi ni fadhila iliyo wazi aliyo tukhusisha sisi Mwenyezi Mungu, "Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri." Sulaiman a.s. ni mwana wa Daudi, naye ni Nabii na Mfalme kama yeye. Aliishi mnamo mwaka 974 mpaka 937 K.K. (yaani Kabla ya Kuzaliwa Nabii Isa). Mwenyezi Mungu alimjaalia kumjuvya kufahamu maneno ya ndege. Uchunguzi wa kisasa umeonyesha kwamba kila namna ya ndege wana njia zao za kufahamiana wao kwa wao. Katika njia hizo ni kwa kugusa, na sauti, na ishara.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَحُشِرَ لِسُلَیۡمَـٰنَ جُنُودُهُۥ مِنَ ٱلۡجِنِّ وَٱلۡإِنسِ وَٱلطَّیۡرِ فَهُمۡ یُوزَعُونَ ﴿١٧﴾

Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu.

Na Sulaiman alikusanya majeshi yake ya majini, watu, na ndege, kwenye uwanja mmoja. Na wao wakawa jeshi moja lenye nidhamu kwa vile kudhibitiwa wa mwanzo mpaka mwisho.


Arabic explanations of the Qur’an:

حَتَّىٰۤ إِذَاۤ أَتَوۡاْ عَلَىٰ وَادِ ٱلنَّمۡلِ قَالَتۡ نَمۡلَةࣱ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلنَّمۡلُ ٱدۡخُلُواْ مَسَـٰكِنَكُمۡ لَا یَحۡطِمَنَّكُمۡ سُلَیۡمَـٰنُ وَجُنُودُهُۥ وَهُمۡ لَا یَشۡعُرُونَ ﴿١٨﴾

Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua.

Hata walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, mdudu chungu mmoja akasema: Enyi wadudu chungu! Ingieni vishimoni mwenu, asije Sulaiman na askari wake wakakuuweni na wao wala hawahisi kuwa nyinyi mpo. "Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua." Inafahamikana wazi katika Aya hii kuwa wadudu chungu wanaishi kwa makundi, yaani wana umoja, na moja katika sifa zao ni kuwa macho na kutahadhari. Na inajuulikana tangu zamani kuwa wadudu chungu wana sifa kadhaa wa kadhaa makhsusi ambazo zinaonyesha kuwa wana umoja wenye nidhamu madhubuti katika hukumu, na wana kiasi kikubwa cha akili, na werevu, na nguvu za kukumbuka, na kupenda kazi na kukakamia, na juhudi isiyo jua kunyong'onyea wala kukata tamaa. Kama wanavyo juulikana kuwa wana wingi wa hila za kuendesha kazi zao. Na dalili ya hayo ni kuwa jamaa wa wadudu chungu ni peke yao baada ya binaadamu ndio wanao zika maiti wao. Na makundi mbali mbali yao yanashughulikia kukutana pahala pamoja kwa nyakati maalumu. Kwa ajili ya hayo zimewekwa siku makhsusi za kusimamisha soko wanapo kusanyika makundi yote kwa kubadilishana bidhaa na kujuana. Na makundi haya yanapo kutana hutokea mazungumzo kwa hima kubwa, na huulizana masuala yaliyo khusiana na mambo yao. Katika yanayo onekana yaliyo fungamana na mikusanyiko hiyo ni kuzuka mashauri yaliyo khusu umma wao, kama kutengeneza barabara ndefu, kwa subira na kukakamia kunako staajabisha. Wala makundi haya hayatosheki na kufanya kazi mchana tu, bali huendeleza kazi zao katika masiku ya mbaamwezi; ama masiku ya kiza hubaki mwahala mwao. Na jamaa wa makundi haya wana njia za pekee za kukusanya na kubeba na kuhifadhi vifaa vyao vya kula. Akishindwa mdudu kuchukua chakula alicho kikusanya kwa mdomo wake hukisukuma kwa miguu yake ya nyuma, na akakinyanyua kwa mikono yake. Na katika mtindo wao ni kuzing'ong'ona mbegu, na kuzipasua baadhi ya nafaka kabla ya kuzirindika ili zisije kuchipua. Na mbegu kubwa kubwa huzigawa vipande vipande ili iwe wepesi kuziingiza katika ghala zao. Na pindi zikiroana kwa mvua huzitoa zipate upepo na jua zikauke.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَتَبَسَّمَ ضَاحِكࣰا مِّن قَوۡلِهَا وَقَالَ رَبِّ أَوۡزِعۡنِیۤ أَنۡ أَشۡكُرَ نِعۡمَتَكَ ٱلَّتِیۤ أَنۡعَمۡتَ عَلَیَّ وَعَلَىٰ وَ ٰ⁠لِدَیَّ وَأَنۡ أَعۡمَلَ صَـٰلِحࣰا تَرۡضَىٰهُ وَأَدۡخِلۡنِی بِرَحۡمَتِكَ فِی عِبَادِكَ ٱلصَّـٰلِحِینَ ﴿١٩﴾

Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema.

Sulaiman akatabasamu akicheka kwa ile kauli ya mdudu chungu yenye kushughulikia maslaha yao, na akahisi neema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo juu yake. Akasema: Ewe Uliye niumba! Nijaalie niwe na shukrani kwako kwa neema ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na niwezeshe nitende vitendo vyema unavyo viridhia, na unitie kwenye rehema yako iliyo timia.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَتَفَقَّدَ ٱلطَّیۡرَ فَقَالَ مَا لِیَ لَاۤ أَرَى ٱلۡهُدۡهُدَ أَمۡ كَانَ مِنَ ٱلۡغَاۤىِٕبِینَ ﴿٢٠﴾

Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu?

Akalikagua jeshi lake la ndege asimwone Hud-hud. Akastaajabu, akasema: Mbona simwoni Hud-hud! Yupo hapa na mimi simwoni, au ameghibu hayupo miongoni mwetu?


Arabic explanations of the Qur’an:

لَأُعَذِّبَنَّهُۥ عَذَابࣰا شَدِیدًا أَوۡ لَأَاْذۡبَحَنَّهُۥۤ أَوۡ لَیَأۡتِیَنِّی بِسُلۡطَـٰنࣲ مُّبِینࣲ ﴿٢١﴾

Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee hoja ya kutosha.

Wallahi! Nitampatisha adhabu kali ya kumshikisha adabu, au nitamchinja ikiwa kosa lake ni kubwa! Ila aniletee hoja madhubuti ya kumtoa makosani kwa kuto kuwepo mbele yangu.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَمَكَثَ غَیۡرَ بَعِیدࣲ فَقَالَ أَحَطتُ بِمَا لَمۡ تُحِطۡ بِهِۦ وَجِئۡتُكَ مِن سَبَإِۭ بِنَبَإࣲ یَقِینٍ ﴿٢٢﴾

Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini.

Na Hud-hud alikuwa kakaa si pahala mbali kwa muda usio kuwa mrefu. Kisha akamjia Sulaiman, akamwambia: Nimejua jambo ulilo kuwa wewe hujalijua, na nimekujia kutoka nchi ya Sabai na khabari muhimu sana, nayo ni ya kweli kwa yakini. "Basi hakukaa mbali, na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka." Hizi ndizo Aya khasa zilizo khusu Ufalme wa Sabai. Na hii Sabai ni moja katika falme za kusini ya Arabuni, inayo itwa Yaman, na ambayo zamani ilikuwa ni maarufu kwa jina la "Arabia Iliyo Neemeka". Na jina hili la mwisho linaonyesha maendeleo yake na utajiri wake. Kwani kwa hakika ilikuwa nchi hiyo ina ustaarabu wa juu tangu miaka elfu mbili kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. Ikitegemea makulima, kwa sababu ya rutuba ya ardhi yake, na uzuri wa hali yake ya hewa. Na pia ikitegemea biashara kwa kuwa ipo kati baina ya Bara Hindi, na Uhabeshi, na Somalia, na Sham, na Iraq. Na kwa hakika mahodhi yaliyo jengwa kuwekea maji na kuyatumia, na maarufu yao yote ni Hodhi Maa'rib (Tazama Aya 16 Surat Sabai) na miji iliyo jengewa ngome, na makasri, na mahekalu, yanashuhudia mpaka hii leo maendeleo ya kijamii ya utajiri ulio kuwako katika nchi hii. Na hakika nakshi walizo zinakishi watawala wao, na baina ya nakshi hizo zipo kanuni za kuendesha mambo ya ujenzi na mengineyo, yanaonyesha kwa kila dalili ukomo wa ustaarabu ulio nawiri walio ufikilia. Na huu ufalme wa Sabai ambao ulifikilia kilele cha kustawi kwake katika siku za Sulaiman a.s. kiasi ya karne kumi kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. ulikuwa ni ufalme kama wa kabla yake, yaani watoto wakiwarithi baba zao. Na kwa hivyo alikuwa akihukumu wakati wa Sulaiman a.s. Malkia. Wataalamu wa taarikhi wamekhitalifiana juu ya jina la Malkia huyo. Waarabu wakimwita Balqiis; akisaidiwa na wazee wahishimiwa kama ni Baraza la Mashauri lake. (Tazama Aya 28-33 katika Surat An-naml.) Wala haikuthibitisha taarikh (historia) kuwa Ufalme wa Sabai ulikuwa dola ya kuteka nchi, bali ulikuwa ufalme wa biashara, na misafara. Katika mabaki yake hatuoni kutajwa vita au kuteka nchi isipo kuwa kwa uchache. Na haya ni kuwa umuhimu wa majeshi yake ulikuwa ni kuhifadhi ngome zake na kuzihami, na kulinda misafara yake kwa aghlabu. Na wananchi wa Sabai walikuwa ni mapagani, makafiri, wakiliabudu jua, kama ilivyo kuja katika Aya tukufu nambari 24 katika Sura hii. Pia wakiabudu mwezi. Na hao ndio miungu yao muhimu kabisa. Na walikuwa wakiwatolea sadaka na wakifukiza ubani katika mahekalu yao.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنِّی وَجَدتُّ ٱمۡرَأَةࣰ تَمۡلِكُهُمۡ وَأُوتِیَتۡ مِن كُلِّ شَیۡءࣲ وَلَهَا عَرۡشٌ عَظِیمࣱ ﴿٢٣﴾

Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.

Hakika mimi nimewaona watu wa Sabai wanatawaliwa na mwanamke, na amepewa kila kheri za kidunia, naye ana kiti cha enzi kikubwa kinacho onyesha dalili ya utukufu wa ufalme na nguvu za madaraka yake.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَجَدتُّهَا وَقَوۡمَهَا یَسۡجُدُونَ لِلشَّمۡسِ مِن دُونِ ٱللَّهِ وَزَیَّنَ لَهُمُ ٱلشَّیۡطَـٰنُ أَعۡمَـٰلَهُمۡ فَصَدَّهُمۡ عَنِ ٱلسَّبِیلِ فَهُمۡ لَا یَهۡتَدُونَ ﴿٢٤﴾

Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka

Nimemwona yeye na watu wake wanaabudu jua, wala hawamuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani amewazainishia vitendo vyao na wenyewe wakaviona ni vizuri na hali ni viovu. Kwa hivyo amewapoteza Njia ya Haki, basi hawakuongoka.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَلَّا یَسۡجُدُواْ لِلَّهِ ٱلَّذِی یُخۡرِجُ ٱلۡخَبۡءَ فِی ٱلسَّمَـٰوَ ٰ⁠تِ وَٱلۡأَرۡضِ وَیَعۡلَمُ مَا تُخۡفُونَ وَمَا تُعۡلِنُونَ ﴿٢٥﴾

Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.

Hawamsujudii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye anayafichua yaliyo fichika katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo fanya kwa siri na kwa dhaahiri.


Arabic explanations of the Qur’an:

ٱللَّهُ لَاۤ إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ ٱلۡعَرۡشِ ٱلۡعَظِیمِ ۩ ﴿٢٦﴾

Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi tukufu

Mwenyezi Mungu, ambaye hapana wa kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye, ndiye Mwenye madaraka makuu yasio na ukomo juu ya kila kiumbe.


Arabic explanations of the Qur’an:

۞ قَالَ سَنَنظُرُ أَصَدَقۡتَ أَمۡ كُنتَ مِنَ ٱلۡكَـٰذِبِینَ ﴿٢٧﴾

Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.

Sulaiman akasema kumwambia Hud-hud: Tutaichungua khabari yako hii tujue kwamba umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.


Arabic explanations of the Qur’an:

ٱذۡهَب بِّكِتَـٰبِی هَـٰذَا فَأَلۡقِهۡ إِلَیۡهِمۡ ثُمَّ تَوَلَّ عَنۡهُمۡ فَٱنظُرۡ مَاذَا یَرۡجِعُونَ ﴿٢٨﴾

Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.

Nenda na barua yangu hii umfikishie yeye na kaumu yake. Kisha jitenge nao ujifiche pahali karibu, uangalie wanarejesheana maneno gani.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَتۡ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلۡمَلَؤُاْ إِنِّیۤ أُلۡقِیَ إِلَیَّ كِتَـٰبࣱ كَرِیمٌ ﴿٢٩﴾

(Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa barua tukufu.

Barua ikamfikia yule Malkia, naye basi akawakusanya wahishimiwa wa kaumu yake, na halmashauri wake. Naye akasema: Enyi wahishimiwa! Mimi hakika imenifikilia barua yenye shani kuu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّهُۥ مِن سُلَیۡمَـٰنَ وَإِنَّهُۥ بِسۡمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحۡمَـٰنِ ٱلرَّحِیمِ ﴿٣٠﴾

Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Kisha akawasomea hiyo barua, nayo imeanzia kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na neema zote, ambaye daima anawamiminia waja wake rehema zake.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَلَّا تَعۡلُواْ عَلَیَّ وَأۡتُونِی مُسۡلِمِینَ ﴿٣١﴾

Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye kusalimu amri.

Msifanye kiburi juu yangu, na nijieni nanyi mmet'ii na wanyenyekevu.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَتۡ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلۡمَلَؤُاْ أَفۡتُونِی فِیۤ أَمۡرِی مَا كُنتُ قَاطِعَةً أَمۡرًا حَتَّىٰ تَشۡهَدُونِ ﴿٣٢﴾

Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.

Akaiambia baraza ya washauri wake: Nibainishieni lifaalo katika haya mambo muhimu nilio wekewa mbele yangu. Kwani mimi sikati shauri juu ya jambo lolote mpaka muwe nyinyi mmehudhuria.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالُواْ نَحۡنُ أُوْلُواْ قُوَّةࣲ وَأُوْلُواْ بَأۡسࣲ شَدِیدࣲ وَٱلۡأَمۡرُ إِلَیۡكِ فَٱنظُرِی مَاذَا تَأۡمُرِینَ ﴿٣٣﴾

Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.

Wakamwambia nao wametua: Sisi ni watu wenye nguvu za mwili, na tuna moyo na mashujaa. Hatuogopi vita. Basi angalia wewe jambo unalo taka kutuamrisha nasi ni wenye kut'ii.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَتۡ إِنَّ ٱلۡمُلُوكَ إِذَا دَخَلُواْ قَرۡیَةً أَفۡسَدُوهَا وَجَعَلُوۤاْ أَعِزَّةَ أَهۡلِهَاۤ أَذِلَّةࣰۚ وَكَذَ ٰ⁠لِكَ یَفۡعَلُونَ ﴿٣٤﴾

Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.

Akasema kwa taratibu na kupendelea salama: Hakika watawala wakiingia katika miji mikubwa pamoja na majeshi yao huifisidi, wakaondoa matengenezo yake, wakateketeza makulima na roho, na wakawafanya walio watukufu katika watu wa hiyo miji kuwa ndio madhalili, na huo ndio mtindo wao daima.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنِّی مُرۡسِلَةٌ إِلَیۡهِم بِهَدِیَّةࣲ فَنَاظِرَةُۢ بِمَ یَرۡجِعُ ٱلۡمُرۡسَلُونَ ﴿٣٥﴾

Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi nayo wajumbe.

Na mimi kwa kupendelea salama na uzima nitampelekea zawadi Sulaiman na kaumu yake, na nitatazama wajumbe watarejea na nini - wataikubali zawadi au watairudisha?


Arabic explanations of the Qur’an:

فَلَمَّا جَاۤءَ سُلَیۡمَـٰنَ قَالَ أَتُمِدُّونَنِ بِمَالࣲ فَمَاۤ ءَاتَىٰنِۦَ ٱللَّهُ خَیۡرࣱ مِّمَّاۤ ءَاتَىٰكُمۚ بَلۡ أَنتُم بِهَدِیَّتِكُمۡ تَفۡرَحُونَ ﴿٣٦﴾

Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.

Wajumbe walifika kwa Sayyidina Sulaiman na zawadi zao. Huku anazijua neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu zilio juu yake, Akawaambia naye ndio anamsemeza huyo Malkia na watu wake katika mkabala na wajumbe: Hivyo ndio mnanipa mimi mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ya Unabii, na ufalme, na neema, ni makubwa zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Bali nyinyi kwa hizi zawadi zenu na wingi wa mali yenu mnafurahi, sio kama mimi. Kwa sababu nyinyi hamjui ila yaliyo shikamana na dunia hii tu.


Arabic explanations of the Qur’an:

ٱرۡجِعۡ إِلَیۡهِمۡ فَلَنَأۡتِیَنَّهُم بِجُنُودࣲ لَّا قِبَلَ لَهُم بِهَا وَلَنُخۡرِجَنَّهُم مِّنۡهَاۤ أَذِلَّةࣰ وَهُمۡ صَـٰغِرُونَ ﴿٣٧﴾

Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.

Akasema, akimsemeza yule msemaji kwa jina lao: Ewe mjumbe! Rejea kwao. Wallahi! tutawatokea kwa majeshi wasio yaweza kupambana nayo na kuyakabili. Na tutawatoa kwenye nchi ya Sabai nao wamepoteza utukufu wao, wamefanywa watumwa.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلۡمَلَؤُاْ أَیُّكُمۡ یَأۡتِینِی بِعَرۡشِهَا قَبۡلَ أَن یَأۡتُونِی مُسۡلِمِینَ ﴿٣٨﴾

Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.

Sulaiman akawaelekea binaadamu na majini aliyo dhalilishiwa na Mwenyezi Mungu kumtumikia, akawashitua kwa jambo geni. Akasema: Ni nani katika nyinyi anaweza kuniletea kiti chake cha enzi kikubwa kabla hawajanijia nao wamekwisha nyenyekea wanat'ii.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَ عِفۡرِیتࣱ مِّنَ ٱلۡجِنِّ أَنَا۠ ءَاتِیكَ بِهِۦ قَبۡلَ أَن تَقُومَ مِن مَّقَامِكَۖ وَإِنِّی عَلَیۡهِ لَقَوِیٌّ أَمِینࣱ ﴿٣٩﴾

Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu.

Mmoja pandikizi la kijini lilisema: Mimi nitakuletea, na wewe umekaa katika baraza yako hii, kabla hujaondoka. Na mimi hakika naweza hayo, na muaminifu katika maneno yangu na vitendo vyangu.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَ ٱلَّذِی عِندَهُۥ عِلۡمࣱ مِّنَ ٱلۡكِتَـٰبِ أَنَا۠ ءَاتِیكَ بِهِۦ قَبۡلَ أَن یَرۡتَدَّ إِلَیۡكَ طَرۡفُكَۚ فَلَمَّا رَءَاهُ مُسۡتَقِرًّا عِندَهُۥ قَالَ هَـٰذَا مِن فَضۡلِ رَبِّی لِیَبۡلُوَنِیۤ ءَأَشۡكُرُ أَمۡ أَكۡفُرُۖ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا یَشۡكُرُ لِنَفۡسِهِۦۖ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّی غَنِیࣱّ كَرِیمࣱ ﴿٤٠﴾

Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.

Akasema aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kiti cha enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza aliyo yasema. Sulaiman alipo kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya mtingisiko, alisema: Haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba na akanipa kheri zake ili anifanyie mtihani, nitashukuru kwa neema hizi au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi huyo hakika amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na mwenye kuacha kushukuru kwa neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si mwenye kuhitajia shukrani. Naye ni Karimu wa kuneemesha.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَ نَكِّرُواْ لَهَا عَرۡشَهَا نَنظُرۡ أَتَهۡتَدِیۤ أَمۡ تَكُونُ مِنَ ٱلَّذِینَ لَا یَهۡتَدُونَ ﴿٤١﴾

Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone ataongoka, au atakuwa miongoni mwa wasio ongoka.

Sulaiman akawaambia watu wake: Kigeuzeni geuzeni hichi kiti cha enzi kwa baadhi ya mabadiliko ya nje, tupate kuona atakijua kwa kukiendea au hato kijua na kwa hivyo hato kiendea.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَلَمَّا جَاۤءَتۡ قِیلَ أَهَـٰكَذَا عَرۡشُكِۖ قَالَتۡ كَأَنَّهُۥ هُوَۚ وَأُوتِینَا ٱلۡعِلۡمَ مِن قَبۡلِهَا وَكُنَّا مُسۡلِمِینَ ﴿٤٢﴾

Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake wakasema): Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu.

Alipo fika jicho lake lilipiga kwenye kiti chake cha enzi. Akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni mfano wa hiki? Akasema kwa vile kilivyo kamilika kufanana: Kama kwamba ndicho hichi. Na Sulaiman na walio pamoja naye wakasema: Sisi tulisha pewa ujuzi kumjua Mwenyezi Mungu na uwezo wake na ukweli wa yaliyo kuja kutoka kwake kama anavyo jua mwanamke huyu. Na sisi tangu hapo ni watu tulio mfuata Mwenyezi Mungu na tunamsafia Yeye ibada.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَصَدَّهَا مَا كَانَت تَّعۡبُدُ مِن دُونِ ٱللَّهِۖ إِنَّهَا كَانَتۡ مِن قَوۡمࣲ كَـٰفِرِینَ ﴿٤٣﴾

Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri.

Na zile ibada za jua na mfano wake zilimzuia yule Malkia kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwani yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.


Arabic explanations of the Qur’an:

قِیلَ لَهَا ٱدۡخُلِی ٱلصَّرۡحَۖ فَلَمَّا رَأَتۡهُ حَسِبَتۡهُ لُجَّةࣰ وَكَشَفَتۡ عَن سَاقَیۡهَاۚ قَالَ إِنَّهُۥ صَرۡحࣱ مُّمَرَّدࣱ مِّن قَوَارِیرَۗ قَالَتۡ رَبِّ إِنِّی ظَلَمۡتُ نَفۡسِی وَأَسۡلَمۡتُ مَعَ سُلَیۡمَـٰنَ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِینَ ﴿٤٤﴾

Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo liona alidhani ni maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman) akasema: Hakika hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja na Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Baada ya hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja wake wa ndani ulikuwa umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki wakiogelea humo. Kupandisha nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa alidhania ni maji. Sulaiman akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri yale madhaahiri ya kilimwengu, na akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman. Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu kwa kughurika na ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea pamoja na Sulaiman kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu wote na kuwalea na kuwasimamia.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَلَقَدۡ أَرۡسَلۡنَاۤ إِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمۡ صَـٰلِحًا أَنِ ٱعۡبُدُواْ ٱللَّهَ فَإِذَا هُمۡ فَرِیقَانِ یَخۡتَصِمُونَ ﴿٤٥﴾

. Na kwa kina Thamud tulimtuma ndugu yao Swaleh kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayo gombana.

Na tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh kuwafunza wamuamini Mwenyezi Mungu pekee. Wao wakakimbilia kugombana na kukhitalifiana. Wakawa makundi mawili. Moja lenye kuamini, na moja la kikafiri.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَ یَـٰقَوۡمِ لِمَ تَسۡتَعۡجِلُونَ بِٱلسَّیِّئَةِ قَبۡلَ ٱلۡحَسَنَةِۖ لَوۡلَا تَسۡتَغۡفِرُونَ ٱللَّهَ لَعَلَّكُمۡ تُرۡحَمُونَ ﴿٤٦﴾

Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?

Swaleh akasema nao kuwanasihi: Enyi watu! Mbona mnaihimiza adhabu mlio ahidiwa kabla ya kutubu? Kwa nini hamwombi msamaha kwa Mola wenu Mlezi, mkamuamini Yeye kwa kutaraji akurehemuni?


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالُواْ ٱطَّیَّرۡنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَۚ قَالَ طَـٰۤىِٕرُكُمۡ عِندَ ٱللَّهِۖ بَلۡ أَنتُمۡ قَوۡمࣱ تُفۡتَنُونَ ﴿٤٧﴾

Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni watu mnao jaribiwa.

Wakasema: Sisi tunakuona wewe na hao walio nawe ni wakorofi, ndio tukapatilizwa na ukame. Yeye akasema: Sababu za kheri na shari zinazo kuteremkieni bila ya shaka yoyote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi ni watu mnao pewa mitihani ya neema na nakama, ili mpate kuamini.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَكَانَ فِی ٱلۡمَدِینَةِ تِسۡعَةُ رَهۡطࣲ یُفۡسِدُونَ فِی ٱلۡأَرۡضِ وَلَا یُصۡلِحُونَ ﴿٤٨﴾

Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha.

Na waongozi wa shari kati yao walikuwa ni tisa, kazi yao ni kufisidi katika nchi kwa maoni yao na madai yao. Wala haukuwa mtindo wao kutenda jema lolote.


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالُواْ تَقَاسَمُواْ بِٱللَّهِ لَنُبَیِّتَنَّهُۥ وَأَهۡلَهُۥ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِیِّهِۦ مَا شَهِدۡنَا مَهۡلِكَ أَهۡلِهِۦ وَإِنَّا لَصَـٰدِقُونَ ﴿٤٩﴾

Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli.

Wale washirikina wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Apishaneni kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwamba kwa yakini tutamshambulia yeye na ahali zake, na tutawauwa. Kisha tutamwambia jamaa yao wa damu kwamba sisi hatukayaona mauwaji yake wala ya ahali zake. Na hakika sisi ni wasema kweli kwa haya tuliyo yataja.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَمَكَرُواْ مَكۡرࣰا وَمَكَرۡنَا مَكۡرࣰا وَهُمۡ لَا یَشۡعُرُونَ ﴿٥٠﴾

Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu, na wao hawatambui.

Walipanga kumuuwa Swaleh na ahali zake, na Mwenyezi Mungu nyuma yao kapanga kumwokoa Nabii wake na ahali zake, na kuwateketeza wao, na hali wao hata hawatambui.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَٱنظُرۡ كَیۡفَ كَانَ عَـٰقِبَةُ مَكۡرِهِمۡ أَنَّا دَمَّرۡنَـٰهُمۡ وَقَوۡمَهُمۡ أَجۡمَعِینَ ﴿٥١﴾

Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote.

Ewe Nabii! Hebu tazama vipi yalikuwa matokeo ya mipango yao na mipango yetu. Sisi tuliwaangamiza wote hao wao na kaumu yao.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَتِلۡكَ بُیُوتُهُمۡ خَاوِیَةَۢ بِمَا ظَلَمُوۤاْۚ إِنَّ فِی ذَ ٰ⁠لِكَ لَـَٔایَةࣰ لِّقَوۡمࣲ یَعۡلَمُونَ ﴿٥٢﴾

Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua.

Na hebu yatazame mabaki yao. Utakuta nyumba zao zimeanguka, zimevurugika, kwa sababu ya udhalimu wao na kufru zao, na kumtakia shari Nabii wao. Hakika kwa walio fanyiwa kina Thamud ipo Ishara kwa watu wanao ujua uwezo wetu na wakawaidhika.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَأَنجَیۡنَا ٱلَّذِینَ ءَامَنُواْ وَكَانُواْ یَتَّقُونَ ﴿٥٣﴾

Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa wanamchamngu.

Na Sisi tukakiokoa kikundi kilicho muamini Saleh kutokana na hilaki hii, na wakawa wanao gopa kuziacha amri zake.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَلُوطًا إِذۡ قَالَ لِقَوۡمِهِۦۤ أَتَأۡتُونَ ٱلۡفَـٰحِشَةَ وَأَنتُمۡ تُبۡصِرُونَ ﴿٥٤﴾

Na Luut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya uchafu nanyi mnaona?

Ewe Nabii! Mtaje Luut'i na khabari zake pamoja na kaumu ya watendao uchafu, pale alipo waambia: Je! Mnafanya dhambi hizi ambazo zimepita hadi ya uchafu na kinyume na maumbile, na hali nyinyi mnaona na mnaangalia uovu wa haya mliyo yashikilia?


Arabic explanations of the Qur’an:

أَىِٕنَّكُمۡ لَتَأۡتُونَ ٱلرِّجَالَ شَهۡوَةࣰ مِّن دُونِ ٱلنِّسَاۤءِۚ بَلۡ أَنتُمۡ قَوۡمࣱ تَجۡهَلُونَ ﴿٥٥﴾

Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio badala ya wanawake? Hakika nyinyi ni watu mnao fanya ujinga kabisa!

Hivyo inaelekea katika nadhari ya akili zenu na maumbile kuwaingilia wanaume kwa matamanio yenu, na mkwawacha wanawake? Ama kweli nyinyi mmesibiwa na upumbavu na ujinga wa kufudikiza, hata imekuwa hamwezi tena kuteuwa baina ya kiovu na chema.


Arabic explanations of the Qur’an:

۞ فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوۡمِهِۦۤ إِلَّاۤ أَن قَالُوۤاْ أَخۡرِجُوۤاْ ءَالَ لُوطࣲ مِّن قَرۡیَتِكُمۡۖ إِنَّهُمۡ أُنَاسࣱ یَتَطَهَّرُونَ ﴿٥٦﴾

Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Wafukuzeni wafwasi wa Luut'i katika mji wenu. Hao ni watu wanao jitia usafi.

Haikuwa jawabu ya watu wake alipo wakataza ila ni kusema: Mtoleeni mbali Luut'i na wafwasi wake katika mji huu. Kwani wao wanajitakasa hawataki kushirikiana nasi katika haya tuyatendayo.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَأَنجَیۡنَـٰهُ وَأَهۡلَهُۥۤ إِلَّا ٱمۡرَأَتَهُۥ قَدَّرۡنَـٰهَا مِنَ ٱلۡغَـٰبِرِینَ ﴿٥٧﴾

Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe; tukamkadiria katika walio baki nyuma.

Basi Sisi tukamwokoa yeye na ahali zake na ile adhabu walio pelekewa wale watu, isipo kuwa mkewe. Mwenyezi Mungu alimkadiria awe na walio baki nyuma ili apate kuangamia kwa adhabu pamoja na makafiri.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَأَمۡطَرۡنَا عَلَیۡهِم مَّطَرࣰاۖ فَسَاۤءَ مَطَرُ ٱلۡمُنذَرِینَ ﴿٥٨﴾

Na tukawanyeshea mvua. Ni ovu kweli kweli hiyo mvua ya walio kwisha onywa.

Na Sisi tukawanyeshea mvua hao mafisadi, mvua ya adhabu na nakama. Ilikuwa mvua ya kuwahiliki walio onywa kuwa watapata adhabu chungu, na wala wasisikie.


Arabic explanations of the Qur’an:

قُلِ ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ وَسَلَـٰمٌ عَلَىٰ عِبَادِهِ ٱلَّذِینَ ٱصۡطَفَىٰۤۗ ءَاۤللَّهُ خَیۡرٌ أَمَّا یُشۡرِكُونَ ﴿٥٩﴾

Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni bora, au wale wanao washirikisha naye?

Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi namhimidi Mwenyezi Mungu na namsifu Yeye peke yake. Na namwomba Mwenyezi Mungu salama na maamkio kwa waja wake alio wateuwa kwa kuwapa Ujumbe wake. Na ewe Mtume! Waambie washirikina: Je! Kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, Aliye Mpweke, ni bora kwa mwenye kuamini, au kuabudu masanamu mnayo mshirikisha naye, nayo hayawezi kukudhuruni wala kukufaeni?


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمَّنۡ خَلَقَ ٱلسَّمَـٰوَ ٰ⁠تِ وَٱلۡأَرۡضَ وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ ٱلسَّمَاۤءِ مَاۤءࣰ فَأَنۢبَتۡنَا بِهِۦ حَدَاۤىِٕقَ ذَاتَ بَهۡجَةࣲ مَّا كَانَ لَكُمۡ أَن تُنۢبِتُواْ شَجَرَهَاۤۗ أَءِلَـٰهࣱ مَّعَ ٱللَّهِۚ بَلۡ هُمۡ قَوۡمࣱ یَعۡدِلُونَ ﴿٦٠﴾

AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu walio potoka.

Bali, ewe Mtume, waulize: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake, na akakuteremshieni kutoka mbinguni mvua yenye manufaa, na kwa hiyo akakuotesheeni bustani nzuri zenye kupendeza. Msingeli weza nyinyi kuiotesha miti yake ya namna mbali mbali, na rangi mbali mbali, na matunda mbali mbali! Mipango hii iliyo umana sawa katika uumbaji inathibitisha kuwa hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Lakini makafiri ni watu walio potoka wakaiacha Haki na Imani, na wameelekea kwenye upotovu na ushirikina.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمَّن جَعَلَ ٱلۡأَرۡضَ قَرَارࣰا وَجَعَلَ خِلَـٰلَهَاۤ أَنۡهَـٰرࣰا وَجَعَلَ لَهَا رَوَ ٰ⁠سِیَ وَجَعَلَ بَیۡنَ ٱلۡبَحۡرَیۡنِ حَاجِزًاۗ أَءِلَـٰهࣱ مَّعَ ٱللَّهِۚ بَلۡ أَكۡثَرُهُمۡ لَا یَعۡلَمُونَ ﴿٦١﴾

Au nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na akajaalia ndani yake mito, na akaweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili kiziwizi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.

Bali waulize, ewe Mtume: Nani aliye itengeneza ardhi hata ikafaa kukaliwa na watu wakatulia humo, na akaumba mito kati yake, na juu yake akaumba milima kuizuilia isiyumbe yumbe, na akayatenganisha maji matamu na maji ya chumvi hata yasichanganyike? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kuumba peke yake. Lakini wengi wa watu hawanafiiki na ujuzi wa Haki kama ilivyo. Wamekuwa kama kwamba hawajui kitu.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمَّن یُجِیبُ ٱلۡمُضۡطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَیَكۡشِفُ ٱلسُّوۤءَ وَیَجۡعَلُكُمۡ خُلَفَاۤءَ ٱلۡأَرۡضِۗ أَءِلَـٰهࣱ مَّعَ ٱللَّهِۚ قَلِیلࣰا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo mwomba, na akaiondoa dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayo yazingatia.

Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye muitikia aliye shikwa na shida katika maombi yake, pale anapo shikwa na shida, akamtegemea Mwenyezi Mungu kwa unyonge na unyenyekevu, naye akamwondolea huyo mtu karaha iliyo msibu, na akakufanyeni warithi wa walio kutangulieni katika nchi? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu wa kukupeni neema zote hizi. Lakini nyinyi makafiri, ni kuchache kabisa kuwaidhika kwenu.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمَّن یَهۡدِیكُمۡ فِی ظُلُمَـٰتِ ٱلۡبَرِّ وَٱلۡبَحۡرِ وَمَن یُرۡسِلُ ٱلرِّیَـٰحَ بُشۡرَۢا بَیۡنَ یَدَیۡ رَحۡمَتِهِۦۤۗ أَءِلَـٰهࣱ مَّعَ ٱللَّهِۚ تَعَـٰلَى ٱللَّهُ عَمَّا یُشۡرِكُونَ ﴿٦٣﴾

Au nani yule anaye kuongoeni katika giza la bara na bahari, na akazipeleka pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya wanao washirikisha naye.

Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye waongoza katika nyendo za katika giza la usiku katika safari za nchi kavu na baharini? Na nani anaye zipeleka pepo zinazo bashiria mvua, nayo ni rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu anaye fanya hayo? Mwenyezi Mungu Subhanahu ametakasika kuwa na mshirika.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمَّن یَبۡدَؤُاْ ٱلۡخَلۡقَ ثُمَّ یُعِیدُهُۥ وَمَن یَرۡزُقُكُم مِّنَ ٱلسَّمَاۤءِ وَٱلۡأَرۡضِۗ أَءِلَـٰهࣱ مَّعَ ٱللَّهِۚ قُلۡ هَاتُواْ بُرۡهَـٰنَكُمۡ إِن كُنتُمۡ صَـٰدِقِینَ ﴿٦٤﴾

Au nani anaye uanzisha uumbaji, kisha akaurejesha? Na nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Sema: Leteni hoja zenu kama nyinyi ni wasema kweli.

Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye anzisha uumbaji tangu mwanzo, na kisha baada ya kupotea kwake akaurejesha kama ulivyo kuwa? Na nani anaye kuteremshieni riziki kutoka mbinguni, na akaitoa kwenye ardhi? Hakuna mungu pamoja na Mwenyezi Mungu atendaye hayo. Sema, ewe Mtume, kuwatahayarisha na kuwakanya: Kama nyinyi mnaye mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu basi tupeni hoja ya hayo, ikiwa mnadai kuwa nyinyi ni wasema kweli. Na wala hayataweza kuwa hayo kwenu.


Arabic explanations of the Qur’an:

قُل لَّا یَعۡلَمُ مَن فِی ٱلسَّمَـٰوَ ٰ⁠تِ وَٱلۡأَرۡضِ ٱلۡغَیۡبَ إِلَّا ٱللَّهُۚ وَمَا یَشۡعُرُونَ أَیَّانَ یُبۡعَثُونَ ﴿٦٥﴾

Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Wala wao hawajui lini watafufuliwa.

Sema, ewe Mtume: Hakika mwenye kutenda yote haya peke yake ndiye Yeye Subhanahu aliye tengeka peke yake kwa kuyajua mambo ya ghaibu yalioko mbinguni na duniani. Na Yeye huyo ndiye Mwenyezi Mungu wa pekee. Wala watu hawajui wakati gani watafufuliwa kutoka makaburini kwao kwa ajili ya kuhisabiwa na kulipwa.


Arabic explanations of the Qur’an:

بَلِ ٱدَّ ٰ⁠رَكَ عِلۡمُهُمۡ فِی ٱلۡـَٔاخِرَةِۚ بَلۡ هُمۡ فِی شَكࣲّ مِّنۡهَاۖ بَلۡ هُم مِّنۡهَا عَمُونَ ﴿٦٦﴾

Kwani huo ujuzi wao umefikilia kuijua Akhera? Bali wao wamo katika shaka nayo tu, bali wao ni vipofu nayo.

Ujuzi wao wa Akhera umefuatana na ujinga, na huo ukawapelekea kuitilia shaka. Nao wamekuwa vipofu hawaitambui Haki katika jambo lolote, kwa sababu upotovu umefisidi fahamu zao.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَقَالَ ٱلَّذِینَ كَفَرُوۤاْ أَءِذَا كُنَّا تُرَ ٰ⁠بࣰا وَءَابَاۤؤُنَاۤ أَىِٕنَّا لَمُخۡرَجُونَ ﴿٦٧﴾

Na wakasema walio kufuru: Tutapo kuwa mchanga, sisi na baba zetu, hivyo kweli tutakuja tolewa?

Wakasema makafiri kwa kukanya kufufuliwa: Hivyo sisi tukisha kuwa mchanga, na ikisha oza miili yetu na ya baba zetu walio tutangulia, ndio tutarejeshwa tutolewe upya tuwe wahai?


Arabic explanations of the Qur’an:

لَقَدۡ وُعِدۡنَا هَـٰذَا نَحۡنُ وَءَابَاۤؤُنَا مِن قَبۡلُ إِنۡ هَـٰذَاۤ إِلَّاۤ أَسَـٰطِیرُ ٱلۡأَوَّلِینَ ﴿٦٨﴾

Haya haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale.

Muhammad ametuahidi kuwa tutafufuliwa, kama Mitume walio tangulia walivyo waahidi baba zetu. Ingeli kuwa hayo ni kweli, basi yangeli kwisha kuwa. Haya si chochote ila ni uwongo tu wa watu wa kale.


Arabic explanations of the Qur’an:

قُلۡ سِیرُواْ فِی ٱلۡأَرۡضِ فَٱنظُرُواْ كَیۡفَ كَانَ عَـٰقِبَةُ ٱلۡمُجۡرِمِینَ ﴿٦٩﴾

Sema: Nendeni katika ardhi, na tazameni ulikuwaje mwisho wa wakosefu.

Ewe Mtume! Waambie: Tembeeni duniani, na mtazame mabaki ya yaliyo wapata walio kadhibisha, nayo ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Huenda labda mkayazingatia haya, na mkaikhofu adhabu ya Akhera.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَلَا تَحۡزَنۡ عَلَیۡهِمۡ وَلَا تَكُن فِی ضَیۡقࣲ مِّمَّا یَمۡكُرُونَ ﴿٧٠﴾

Wala usiwahuzunukie wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya hila zao wanazo zifanya.

Ewe Mtume! Usiwahuzunukie makafiri wasio kufuata. Kwani kwa hakika waajibu wako ni kufikisha Ujumbe tu. Wala usiwe na dhiki kifuani mwako kwa sababu ya hila zao na vitimbi vyao. Kwani hakika Mwenyezi Mungu atakupa ushindi juu yao.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَیَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا ٱلۡوَعۡدُ إِن كُنتُمۡ صَـٰدِقِینَ ﴿٧١﴾

Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa mnasema kweli?

Na makafiri wanafanya ukomo wa juhudi yao kukanusha, na wanaihimiza adhabu kwa kusema: Lini, basi, itakuwa hiyo adhabu ambayo mnatutishia kuwa itakuja, ikiwa nyinyi mnasema kweli kuwa adhabu itawashukia wanao kanusha?


Arabic explanations of the Qur’an:

قُلۡ عَسَىٰۤ أَن یَكُونَ رَدِفَ لَكُم بَعۡضُ ٱلَّذِی تَسۡتَعۡجِلُونَ ﴿٧٢﴾

Sema: Asaa ni karibu kukufikieni sehemu ya yale mnayo yahimiza.

Ewe Mtume! Sema: Huenda ikakukuteni, na imekukaribieni baadhi ya adhabu mnayo ihimiza.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو فَضۡلٍ عَلَى ٱلنَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكۡثَرَهُمۡ لَا یَشۡكُرُونَ ﴿٧٣﴾

Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye fadhila kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.

Na hakika Mwenyezi Mungu Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ni Mwenye neema na hisani kwa watu wote. Na katika rehema zake ni kuakhirisha hiyo adhabu kwa hao wanao kadhibisha. Lakini watu wengi hawaelewi fadhila za Mwenyezi Mungu wala hawamshukuru.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنَّ رَبَّكَ لَیَعۡلَمُ مَا تُكِنُّ صُدُورُهُمۡ وَمَا یُعۡلِنُونَ ﴿٧٤﴾

Na hakika Mola wako Mlezi anayajua yanayo ficha vifua vyao na wanayo yatangaza.

Ewe Mtume! Hakika Mwenyezi Mungu, Mola wako Mlezi, hapana shaka anajua kila wanalo lificha na wanalo litangaza, ikiwa maneno au vitendo viovu. Naye atakuja walipa kwayo.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَمَا مِنۡ غَاۤىِٕبَةࣲ فِی ٱلسَّمَاۤءِ وَٱلۡأَرۡضِ إِلَّا فِی كِتَـٰبࣲ مُّبِینٍ ﴿٧٥﴾

Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu kinacho bainisha.

Na hapana kilicho fichikana cha ghaibu, na kiwe kidogo vipi au duni, mbinguni au katika ardhi ila Mwenyezi Mungu anakijua, na amekidhibiti katika Kitabu cha Haki kilioko kwake.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّ هَـٰذَا ٱلۡقُرۡءَانَ یَقُصُّ عَلَىٰ بَنِیۤ إِسۡرَ ٰ⁠ۤءِیلَ أَكۡثَرَ ٱلَّذِی هُمۡ فِیهِ یَخۡتَلِفُونَ ﴿٧٦﴾

Hakika Qur'ani hii inawasimulia Wana wa Israili mengi wanayo khitalifiana nayo.

Hakika Kitabu hiki alicho teremshiwa Muhammad kinawawekea wazi Wana wa Israili ukweli wa yaliyo kuja katika Taurati, katika mambo ya itikadi na hukumu na hadithi. Na kinawarudisha kwenye kweli katika mambo waliyo khitalifiana kwayo.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنَّهُۥ لَهُدࣰى وَرَحۡمَةࣱ لِّلۡمُؤۡمِنِینَ ﴿٧٧﴾

Nayo hakika ni Uwongofu na Rehema kwa Waumini.

Hakika Kitabu hichi ni Uwongofu wa kuokoa watu wasipotee, na ni Rehema ya kuwakinga na adhabu wote wenye kukiamini.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّ رَبَّكَ یَقۡضِی بَیۡنَهُم بِحُكۡمِهِۦۚ وَهُوَ ٱلۡعَزِیزُ ٱلۡعَلِیمُ ﴿٧٨﴾

Hakika Mola wako Mlezi atawahukumu kwa hukumu yake, naye ni Mwenye nguvu Mjuzi.

Ewe Mtume! Hakika Mola wako Mlezi atawapambanua watu wote Siku ya Kiyama kwa uadilifu wake. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, basi hapana wa kuipinga hukumu yake. Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, basi mbele yake kweli haiwezi kuchanganyika na uwongo.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَتَوَكَّلۡ عَلَى ٱللَّهِۖ إِنَّكَ عَلَى ٱلۡحَقِّ ٱلۡمُبِینِ ﴿٧٩﴾

Basi mtegemee Mweneyezi Mungu; hakika wewe uko juu ya Haki iliyo wazi.

Basi, ewe Mtume, mtegemezee mambo yako Mwenyezi Mungu, na shikilia wito wako kwa kuamini kuwa utashinda tu, kwa sababu wewe uko juu ya Haki iliyo wazi, na mapuuza ya makafiri kukupuuza wewe hakutakudhuru kitu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّكَ لَا تُسۡمِعُ ٱلۡمَوۡتَىٰ وَلَا تُسۡمِعُ ٱلصُّمَّ ٱلدُّعَاۤءَ إِذَا وَلَّوۡاْ مُدۡبِرِینَ ﴿٨٠﴾

Kwa hakika wewe huwezi kuwafanya maiti wasikie, wala kuwafanya viziwi wasikie wito, wanapo kwisha geuka kwenda zao.

Ewe Mtume! Hakika wewe huwezi kuwaongoa hao, kwani hao ni kama maiti kwa kuto tambua kitu, na kama viziwi kwa kutosikia. Basi hao hawako tayari kuusikia wito wako kwa vile walivyo shikilia kukupuuza.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَمَاۤ أَنتَ بِهَـٰدِی ٱلۡعُمۡیِ عَن ضَلَـٰلَتِهِمۡۖ إِن تُسۡمِعُ إِلَّا مَن یُؤۡمِنُ بِـَٔایَـٰتِنَا فَهُم مُّسۡلِمُونَ ﴿٨١﴾

Wala huwezi kuwaongoa vipofu waache upotovu wao. Huwezi kuwafanya wasikie isipo kuwa wenye kuziamini Ishara zetu; na hao ndio wat'iifu.

Na wala huwezi kuwaongoa kwenye Haki wale ambao wamepofuka kuona kwao na kutambua kwao. Na huwezi kumfanya asikie ila mwenye kukubali kuziamini Ishara zetu. Hao ndio wenye kut'ii na wenye kuitikia.


Arabic explanations of the Qur’an:

۞ وَإِذَا وَقَعَ ٱلۡقَوۡلُ عَلَیۡهِمۡ أَخۡرَجۡنَا لَهُمۡ دَاۤبَّةࣰ مِّنَ ٱلۡأَرۡضِ تُكَلِّمُهُمۡ أَنَّ ٱلنَّاسَ كَانُواْ بِـَٔایَـٰتِنَا لَا یُوقِنُونَ ﴿٨٢﴾

Na itapo waangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika ardhi atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana na yakini na Ishara zetu.

Na itapo karibia kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu kuileta Saa ya Kiyama na kuwateremshia makafiri adhabu, Mwenyezi Mungu atawatolea watu mnyama kwenye ardhi atakaye waambia miongoni mwa atakayo sema: Hakika makafiri walikuwa hawaiamini miujiza yetu yote, na pia Siku ya Mwisho. Na hayo waliyo kuwa wakiyakanusha sasa yamekwisha kuwa. Na hichi basi kitisho cha hiyo Saa na yanayo fuatia! Hii ndio tafsiri ya Aya hii kwa dhaahiri ya matamko yake. Na zipo tafsiri mbili nyengine ambazo za hii Aya zinazo weza kuwa: Kwanza ni kuwa makusudio ya "Dabbah" ni yeyote aendaye "yadibbu", katika watu au wengineo. Na hapa inachukuliwa kuwa ni watu, watao kuja kabla ya Kiyama. Na maana yake ni kuwa ikiwateremkia kauli juu yao na adhabu ikathibiti watakuja makundi ya Waumini wakiwaendea, wakienea kote kote, wakizitikisa nguzo za ukafiri. Tafsiri ya pili neno hilo "Dabbah" makusudio yake ni watu waovu, ambao kwa ujinga ni kama wanyama, kama alivyo sema Al As'fahan katika Muqarrarat yake. Na maana yake ni kuwa ikikaribia Siku ya Kiyama, uovu na ufisadi utazidi, na Kiyama wanacho kikanusha makafiri ndio kitakuja. Na hiyo kauli itakuwa, nayo si kauli ya kutamkwa kwa mdomo, lakini kwa kuwa hali yenyewe itakuwa hivyo ni kama iliyo semwa, kama maoni yaliyo kwisha tangulia.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَیَوۡمَ نَحۡشُرُ مِن كُلِّ أُمَّةࣲ فَوۡجࣰا مِّمَّن یُكَذِّبُ بِـَٔایَـٰتِنَا فَهُمۡ یُوزَعُونَ ﴿٨٣﴾

Na Siku tutapo kusanya kutoka kila umma kundi katika wanao kadhibisha Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu.

Na ewe Mtume! Kumbuka siku tutapo wakusanya kutoka kila kundi la wenye kukadhibisha Ishara zetu, nao ni hao waongozi wanao fuatwa. Basi hao watachungwa wawe mbele ya kaumu zao kuendea hisabu na malipo.


Arabic explanations of the Qur’an:

حَتَّىٰۤ إِذَا جَاۤءُو قَالَ أَكَذَّبۡتُم بِـَٔایَـٰتِی وَلَمۡ تُحِیطُواْ بِهَا عِلۡمًا أَمَّاذَا كُنتُمۡ تَعۡمَلُونَ ﴿٨٤﴾

Hata watakapo fika, atasema (Mwenyezi Mungu): Je! Nyinyi si mlizikanusha Ishara zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya nini?

Na pale watakapo simama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu, atasema Subhanahu kuwaambia kwa kuwadhili na kuwabinya: Nyinyi mlizikadhibisha Ishara zangu zote, na mkazikataa bila ya kuzingatia wala kufahamu. Na khasa mlikuwa mkitenda nini nanyi hamkuumbwa kwa upuuzi?


Arabic explanations of the Qur’an:

وَوَقَعَ ٱلۡقَوۡلُ عَلَیۡهِم بِمَا ظَلَمُواْ فَهُمۡ لَا یَنطِقُونَ ﴿٨٥﴾

Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyo dhulumu. Basi hao hawatasema lolote.

Na adhabu itawateremkia kwa sababu ya kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri. Basi watakuwa hawawezi kujilinda wala kutaka udhuru.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَلَمۡ یَرَوۡاْ أَنَّا جَعَلۡنَا ٱلَّیۡلَ لِیَسۡكُنُواْ فِیهِ وَٱلنَّهَارَ مُبۡصِرًاۚ إِنَّ فِی ذَ ٰ⁠لِكَ لَـَٔایَـٰتࣲ لِّقَوۡمࣲ یُؤۡمِنُونَ ﴿٨٦﴾

Je! Hawaoni kwamba sisi tumeufanya usiku ili watulie, na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.

Bila ya shaka wameshuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameufanya usiku ili wapate kupumzika, na akaufanya mchana una mwangaza, wapate kushughulikia kutafuta maisha yao. Hakika katika hayo zipo dalili wazi za Ungu wa Mwenyezi Mungu, na Upweke wake, kwa watu wanao zingatia wakaamini.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَیَوۡمَ یُنفَخُ فِی ٱلصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِی ٱلسَّمَـٰوَ ٰ⁠تِ وَمَن فِی ٱلۡأَرۡضِ إِلَّا مَن شَاۤءَ ٱللَّهُۚ وَكُلٌّ أَتَوۡهُ دَ ٰ⁠خِرِینَ ﴿٨٧﴾

Na Siku litapo pulizwa baragumu, watahangaika waliomo mbinguni na katika ardhi, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni wanyonge.

Na taja, ewe Mtume, Siku atapo puliza Israfil baragumu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na watapo ingiwa kiwewe walioko katika mbingu na katika ardhi kwa kitisho cha mpulizo huo, isipo kuwa huyo ambaye Mwenyezi Mungu atamtuliza na akamhifadhi na kitisho. Na viumbe vyote watakuja kwa Mola wao Mlezi nao ni madhalili.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَتَرَى ٱلۡجِبَالَ تَحۡسَبُهَا جَامِدَةࣰ وَهِیَ تَمُرُّ مَرَّ ٱلسَّحَابِۚ صُنۡعَ ٱللَّهِ ٱلَّذِیۤ أَتۡقَنَ كُلَّ شَیۡءٍۚ إِنَّهُۥ خَبِیرُۢ بِمَا تَفۡعَلُونَ ﴿٨٨﴾

Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo.

Na unaiona, ewe Mtume, milima na unadhani haitaharaki imetulia tu, lakini kwa hakika inakwenda mbio kama mawingu. Na haya ni katika uundaji wa Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu na akakizua. Hakika Yeye, Subhanahu, ni Mwenye kutimia ujuzi wake kwa yote wayatendayo watu, ya ut'iifu na maasi. Naye atawalipa kwayo. "Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo." Aya hii inathibitisha kuwa vitu vyote vinavyo fuata mvutano wa ardhi, kama milima, bahari, na funiko la anga n.k. vinashirikiana na dunia katika mzunguko wake wa kila siku juu ya msumari-kati wake, na mzunguko wake wa kila mwaka kulizunguka jua. Lakini mzunguko huu hauonekani. Ni kama kwenda kwa mawingu angani. Wanao tazama wanayaona, lakini hawasikii sauti yao, wala hawayagusi. Inaonyesha Aya hii tukufu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye tukuka, ameumba ulimwengu na mipango yake ya kuiendeshea. Naye ni Muweza wa kuifanya hii dunia imetulia tu haizunguki juu ya msumari-kati wake, au akaifanya kuzunguka juu ya msumari-kati wake sawa sawa na kuzunguka kwake kulizunguka jua. Na kwa hivyo ingeli kuwa nusu ya dunia imo kizani totoro kwa muda wa miezi sita, na kwa muda wa miezi sita ikawa nusu ya pili imo katika mwangaza moja kwa moja wa mchana. Na haya yangeli pelekea kuharibika mizani ya joto katika dunia yote. Na kwa hivyo uhai ulioko ungeli toweka duniani. Na Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taa'la, ndiye aliye panga mpango huu uliopo kwa rehema yake na huruma zake kwa waja wake. Na juu ya kuwa Aristakhoris, mtaalamu wa ilimu ya falaki wa Iskandaria (Alexandria) katika Misri, aliandika (310-230 K.K.) juu ya kuzunguka dunia wenyewe kwa wenyewe, maandishi haya ya kisayansi ya kale yalikuwa hayajawafikia Waarabu wakati wa Mtume Muhammad s.a.w. au kabla yake. Bali wa mwanzo wa kuashiria mambo haya katika wao alikuwa Albiruni katika mwaka 1000 B.K. (Baada ya Kuzaliwa Nabii Isa), baada ya kuingia kufasiriwa vitabu vya ilimu za zamani kwa lugha ya Kiarabu ulio kuweko katika enzi za Banul Abbas. Basi kutokea haya kwa ulimi wa Mtume Muhammad s.a.w. ambaye aliye kuwa hajapata ilimu hiyo, ni dalili kuwa haya yalifunuliwa kwake na Mwenyezi Mungu.


Arabic explanations of the Qur’an:

مَن جَاۤءَ بِٱلۡحَسَنَةِ فَلَهُۥ خَیۡرࣱ مِّنۡهَا وَهُم مِّن فَزَعࣲ یَوۡمَىِٕذٍ ءَامِنُونَ ﴿٨٩﴾

Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mahangaiko ya Siku hiyo.

Kila mwenye kuleta wema katika dunia, nayo ni Imani na usafi wa ut'iifu, atapata huko Akhera thawabu kubwa kabisa kwa ajili ya aliyo yatanguliza. Na wenye mema haya watasalimika na khofu na kufazaika Siku ya Kiyama.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَمَن جَاۤءَ بِٱلسَّیِّئَةِ فَكُبَّتۡ وُجُوهُهُمۡ فِی ٱلنَّارِ هَلۡ تُجۡزَوۡنَ إِلَّا مَا كُنتُمۡ تَعۡمَلُونَ ﴿٩٠﴾

Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso zao Motoni. Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda?

Na kila mwenye kuleta uovu katika dunia - nao ni shirki na maasia - na akafa na hayo, basi malipo ya kundi hili ni kuwa Mwenyezi Mungu atawasukumiza juu ya nyuso zao katika Moto, na wataambiwa hapo kwa kuwatahayarisha: Hakika hii leo hamlipwi ila kwa sababu ya shirki yenu na maasi yenu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّمَاۤ أُمِرۡتُ أَنۡ أَعۡبُدَ رَبَّ هَـٰذِهِ ٱلۡبَلۡدَةِ ٱلَّذِی حَرَّمَهَا وَلَهُۥ كُلُّ شَیۡءࣲۖ وَأُمِرۡتُ أَنۡ أَكُونَ مِنَ ٱلۡمُسۡلِمِینَ ﴿٩١﴾

Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu aliye ufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea.

Ewe Mtume! Waambie watu: Sikuamrishwa nimuabudu yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mji wa Makka aliye utukuza, na akaufanya mtakatifu wenye amani, usio faa kumwagwa damu ndani yake, wala kuwindwa wanyama wake, wala kukatwa miti yake. Na vitu vyote viliomo ulimwenguni ni vya Mwenyezi Mungu kuvimiliki na kuvitawala, na mimi nimeamrishwa niwe katika wanao mnyenyekea Mwenyezi Mungu.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَأَنۡ أَتۡلُوَاْ ٱلۡقُرۡءَانَۖ فَمَنِ ٱهۡتَدَىٰ فَإِنَّمَا یَهۡتَدِی لِنَفۡسِهِۦۖ وَمَن ضَلَّ فَقُلۡ إِنَّمَاۤ أَنَا۠ مِنَ ٱلۡمُنذِرِینَ ﴿٩٢﴾

Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji.

Na nimeamrishwa nidumishe kuisoma Qur'ani, kwa ibada, na kuzingatia, na kuwaitia watu wafuate yaliomo humo. Basi mwenye kuongoka, akaiamini, na akakufuata wewe, basi kheri ya hayo na malipo yake ni kwa nafsi yake. Na mwenye kupotea asiifuate Haki, na asikufuate wewe, mwambie: Hakika mimi ni Mtume, naonya, na nafikisha Ujumbe tu.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَقُلِ ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ سَیُرِیكُمۡ ءَایَـٰتِهِۦ فَتَعۡرِفُونَهَاۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَـٰفِلٍ عَمَّا تَعۡمَلُونَ ﴿٩٣﴾

Na sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na myatendayo.

Na sema, ewe Mtume: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa neema ya Unabii na Uwongofu. Mwenyezi Mungu atakuonyesheni hapa duniani athari za uwezo wake, na Akhera atakuonyesheni ukweli wa aliyo kwambieni, na mtayajua vilivyo. Wala Mwenyezi Mungu hashindwi kukuhisabieni wala haghafiliki na vitendo vyenu.


Arabic explanations of the Qur’an: