Surah Al-Qalam (The Pen)

Listen

Swahili

Surah Al-Qalam (The Pen) - Aya count 52

نۤۚ وَٱلۡقَلَمِ وَمَا یَسۡطُرُونَ ﴿١﴾

Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo!

Nuun, ndio harufi ya N, iliyo anzia Sura hii ni kama kupinzana na hao wanao kadhibisha, na ili kuwazindua wenye kusadiki. Naapa kwa kalamu wanayo andikia Malaika na wenginewe, na hayo mambo ya kheri na manufaa wanayo yaandika,


Arabic explanations of the Qur’an:

مَاۤ أَنتَ بِنِعۡمَةِ رَبِّكَ بِمَجۡنُونࣲ ﴿٢﴾

Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu.

Hakika wewe, na Mwenyezi Mungu amekuneemesha kwa kukupa Unabii, si mchachefu wa akili, wala mpumbavu wa mawazo.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنَّ لَكَ لَأَجۡرًا غَیۡرَ مَمۡنُونࣲ ﴿٣﴾

Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika.

Na hakika unapata thawabu kubwa zisio katika kwa ajili ya kufikisha Ujumbe.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِیمࣲ ﴿٤﴾

Na hakika wewe una tabia tukufu.

Na hakika wewe bila ya shaka umeshikamana na sifa nzuri kabisa na vitendo vizuri kabisa alivyo kuumba navyo Mwenyezi Mungu.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَسَتُبۡصِرُ وَیُبۡصِرُونَ ﴿٥﴾

Karibu utaona, na wao wataona!

Karibuni hivi, ewe Muhammad, utaona, na makafiri wataona,


Arabic explanations of the Qur’an:

بِأَییِّكُمُ ٱلۡمَفۡتُونُ ﴿٦﴾

Ni nani kati yenu aliye pandwa na wazimu.

Ni nani kati yenu aliye mwenda wazimu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعۡلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِیلِهِۦ وَهُوَ أَعۡلَمُ بِٱلۡمُهۡتَدِینَ ﴿٧﴾

Hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye ajuaye zaidi nani aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.

Hakika Mola wako Mlezi, Yeye ndiye Mwenye kumjua zaidi aliye iacha Njia yake, na Yeye ndiye Mwenye kuwajua zaidi wenye akili walio ongoka kumwendea Yeye.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَلَا تُطِعِ ٱلۡمُكَذِّبِینَ ﴿٨﴾

Basi usiwat'ii wanao kadhibisha.

Basi usiyaache uliyo nayo ya kuwapinga wanao kanusha.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَدُّواْ لَوۡ تُدۡهِنُ فَیُدۡهِنُونَ ﴿٩﴾

Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie.

Wanatamani lau ungeli kuwa laini kwao katika baadhi ya mambo, ili na wao wawe laini kwako, kwa tamaa upate kurudishiana nao. (Neno lililo tumiwa hapo "Tud- hinu fayud-hinuun", maana yake khasa "Upake mafuta na wao wapake mafuta". Kiswahili husema: Kumpaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa. Yaani kumpa sifa za uwongo, kumfanyia unaafiki. Kwa Kiarabu ni "Mudaahana". Kupakana mafuta)


Arabic explanations of the Qur’an:

وَلَا تُطِعۡ كُلَّ حَلَّافࣲ مَّهِینٍ ﴿١٠﴾

Wala usimt'ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa,

Wala usiache mwendo wako ulio nao kwenda kinyume na kila mwingi wa viapo, mtu wa kudharauliwa,


Arabic explanations of the Qur’an:

هَمَّازࣲ مَّشَّاۤءِۭ بِنَمِیمࣲ ﴿١١﴾

Mtapitapi apitae akifitini.

Mtapitapi mwenye kueneza aibu za watu, mwenye kuwasengenya watu, kuwasema kwa siri, mwenye kutwaa maneno baina ya watu kwa sababu ya kuwafisidi,


Arabic explanations of the Qur’an:

مَّنَّاعࣲ لِّلۡخَیۡرِ مُعۡتَدٍ أَثِیمٍ ﴿١٢﴾

Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi,

Mwingi wa kupinga kila la kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi,


Arabic explanations of the Qur’an:

عُتُلِّۭ بَعۡدَ ذَ ٰ⁠لِكَ زَنِیمٍ ﴿١٣﴾

Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu.

Mgumu wa moyo, mwenye tabia ya ukavu, muovu maarufu kwa shari, juu ya sifa hizo mbovu alizo nazo.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَن كَانَ ذَا مَالࣲ وَبَنِینَ ﴿١٤﴾

Ati kwa kuwa ana mali na watoto!

Ati kwa kuwa anajiona yeye ana mali na watoto wengi! Amezikadhibisha Aya zetu na amezipuuza.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِذَا تُتۡلَىٰ عَلَیۡهِ ءَایَـٰتُنَا قَالَ أَسَـٰطِیرُ ٱلۡأَوَّلِینَ ﴿١٥﴾

Anapo somewa Aya zetu, husema: Hizi ni simulizi za uwongo za watu wa zamani!

Akisomewa Qur'ani husema: Hivi ni visa vya uwongo vya watu wa kale!


Arabic explanations of the Qur’an:

سَنَسِمُهُۥ عَلَى ٱلۡخُرۡطُومِ ﴿١٦﴾

Tutamtia kovu juu ya pua yake.

Tutambandika alama juu ya pua yake ya kumganda, apate kufedheheka mbele za watu.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّا بَلَوۡنَـٰهُمۡ كَمَا بَلَوۡنَاۤ أَصۡحَـٰبَ ٱلۡجَنَّةِ إِذۡ أَقۡسَمُواْ لَیَصۡرِمُنَّهَا مُصۡبِحِینَ ﴿١٧﴾

Hakika tumewajaribu hawa kama tulivyo wajaribu wale wenye shamba, walipo apa kwamba watayavuna mazao yake itakapo kuwa asubuhi.

Sisi tumewafanyia mtihani watu wa Makka kwa kuwapa neema, nao wakazikufuru; kama tulivyo wafanyia mtihani hao watu wenye shamba, walipo chukua kiapo kuwa watakwenda vuna mazao ya shamba lao asubuhi mapema,


Arabic explanations of the Qur’an:

وَلَا یَسۡتَثۡنُونَ ﴿١٨﴾

Wala hawakusema: Mungu akipenda!

Wala wasimkumbuke Mwenyezi Mungu, wakafunganisha hilo jambo lao na kupenda kwake.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَطَافَ عَلَیۡهَا طَاۤىِٕفࣱ مِّن رَّبِّكَ وَهُمۡ نَاۤىِٕمُونَ ﴿١٩﴾

Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala!

Basi ikaliteremkia shamba hilo balaa kubwa ilio toka kwa Mola wako Mlezi, na hali wao wamelala.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَأَصۡبَحَتۡ كَٱلصَّرِیمِ ﴿٢٠﴾

Likawa kama usiku wa giza.

Likawa hilo shamba kama usiku wa giza kwa masaibu yalio lifikia.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَتَنَادَوۡاْ مُصۡبِحِینَ ﴿٢١﴾

Asubuhi wakaitana.

Asubuhi wakawa wanaitana:


Arabic explanations of the Qur’an:

أَنِ ٱغۡدُواْ عَلَىٰ حَرۡثِكُمۡ إِن كُنتُمۡ صَـٰرِمِینَ ﴿٢٢﴾

Ya kwamba nendeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna.

Amkeni mapema mwende kondeni kwenu kama mmeazimia kuvuna.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَٱنطَلَقُواْ وَهُمۡ یَتَخَـٰفَتُونَ ﴿٢٣﴾

Basi walikwenda na huku wakinong'onezana,

Wakatoka, nao wakinong'ona kuambizana:


Arabic explanations of the Qur’an:

أَن لَّا یَدۡخُلَنَّهَا ٱلۡیَوۡمَ عَلَیۡكُم مِّسۡكِینࣱ ﴿٢٤﴾

Ya kuwa leo hata masikini mmoja asikuingilieni.

Msimwachie masikini yeyote kukuingilieni leo!


Arabic explanations of the Qur’an:

وَغَدَوۡاْ عَلَىٰ حَرۡدࣲ قَـٰدِرِینَ ﴿٢٥﴾

Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimio hilo.

Wakenda hapo asubuhi mpaka kwenye shamba lao, na azma yao ovu hiyo, na wao ni wenye uwezo kaamili wa kutenda hayo kwa kujigamba kwao.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَلَمَّا رَأَوۡهَا قَالُوۤاْ إِنَّا لَضَاۤلُّونَ ﴿٢٦﴾

Basi walipo liona, wakasema: Hakika tumepotea!

Walipo liona limekuwa jeusi limeungua, walisema nao wamebabaika: Hakika sisi bila ya shaka tumepotea. Hili silo shamba letu!


Arabic explanations of the Qur’an:

بَلۡ نَحۡنُ مَحۡرُومُونَ ﴿٢٧﴾

Bali tumenyimwa!

Bali ndilo shamba letu! Na sisi tumenyimwa!


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالَ أَوۡسَطُهُمۡ أَلَمۡ أَقُل لَّكُمۡ لَوۡلَا تُسَبِّحُونَ ﴿٢٨﴾

Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu?

Alisema aliye kuwa muadilifu wao na mbora wao akiwalaumu: Sikukwambieni mlipo kuwa mnasemezana kuwanyima masikini, hebu hamumkumbuki Mwenyezi Mungu mkaiacha niya yenu?


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالُواْ سُبۡحَـٰنَ رَبِّنَاۤ إِنَّا كُنَّا ظَـٰلِمِینَ ﴿٢٩﴾

Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu.

Wakasema walipo rejea kwenye uwongozi wao: Tunamtakasa Mwenyezi Mungu kuwa katudhulumu kwa yaliyo tusibu. Hakika sisi wenyewe ndio tumejidhulumu kwa makusudio yetu maovu.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَأَقۡبَلَ بَعۡضُهُمۡ عَلَىٰ بَعۡضࣲ یَتَلَـٰوَمُونَ ﴿٣٠﴾

Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao.

Wakawa wanaelekeana wao kwa wao wakilaumiana,


Arabic explanations of the Qur’an:

قَالُواْ یَـٰوَیۡلَنَاۤ إِنَّا كُنَّا طَـٰغِینَ ﴿٣١﴾

Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka!

Wakisema: Huku ni kuhiliki kwetu! Hakika sisi tulikuwa tumepita mipaka katika dhulma zetu.


Arabic explanations of the Qur’an:

عَسَىٰ رَبُّنَاۤ أَن یُبۡدِلَنَا خَیۡرࣰا مِّنۡهَاۤ إِنَّاۤ إِلَىٰ رَبِّنَا رَ ٰ⁠غِبُونَ ﴿٣٢﴾

Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.

Asaa Mola wetu Mlezi akatupa badala lilio bora kuliko hili shamba letu. Hakika sisi tunamtaka Mola wetu Mlezi peke yake atupe msamaha na malipo.


Arabic explanations of the Qur’an:

كَذَ ٰ⁠لِكَ ٱلۡعَذَابُۖ وَلَعَذَابُ ٱلۡـَٔاخِرَةِ أَكۡبَرُۚ لَوۡ كَانُواْ یَعۡلَمُونَ ﴿٣٣﴾

Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangeli jua!

Mfano wa kama hayo yaliyo yasibu hilo shamba ndio inakuwa adhabu yangu ninayo iteremsha duniani kwa anaye stahiki. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi lau kuwa watu wanajua hayo.


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّ لِلۡمُتَّقِینَ عِندَ رَبِّهِمۡ جَنَّـٰتِ ٱلنَّعِیمِ ﴿٣٤﴾

Hakika wachamngu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi.

Hakika wachamngu watapata kwa Mola wao Mlezi Bustani za neema safi.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَفَنَجۡعَلُ ٱلۡمُسۡلِمِینَ كَٱلۡمُجۡرِمِینَ ﴿٣٥﴾

Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu?

Je! Sisi tudhulumu katika hukumu yetu, tuwafanye Waislamu sawa na makafiri?


Arabic explanations of the Qur’an:

مَا لَكُمۡ كَیۡفَ تَحۡكُمُونَ ﴿٣٦﴾

Mna nini? Mnahukumu vipi?

Vipi mnahukumia mfano wa hukumu kama hii ya dhulma?


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمۡ لَكُمۡ كِتَـٰبࣱ فِیهِ تَدۡرُسُونَ ﴿٣٧﴾

Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma?

Kwani mnacho kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu mnacho kisoma,


Arabic explanations of the Qur’an:

إِنَّ لَكُمۡ فِیهِ لَمَا تَخَیَّرُونَ ﴿٣٨﴾

Kuwa mtapata humo mnayo yapenda?

Na humo yamo hayo mnayo yapenda?


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمۡ لَكُمۡ أَیۡمَـٰنٌ عَلَیۡنَا بَـٰلِغَةٌ إِلَىٰ یَوۡمِ ٱلۡقِیَـٰمَةِ إِنَّ لَكُمۡ لَمَا تَحۡكُمُونَ ﴿٣٩﴾

Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayo jihukumia?

Au kwani mnazo ahadi juu yetu zenye kutiliwa mkazo kwa viapo, zenye kubaki mpaka Siku ya Kiyama, kwamba mnayo haki ya hayo mnayo jihukumia?


Arabic explanations of the Qur’an:

سَلۡهُمۡ أَیُّهُم بِذَ ٰ⁠لِكَ زَعِیمٌ ﴿٤٠﴾

Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya?

Ewe Muhammad! Waulize washirikina: Ni nani dhamini wa hukumu hiyo?


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمۡ لَهُمۡ شُرَكَاۤءُ فَلۡیَأۡتُواْ بِشُرَكَاۤىِٕهِمۡ إِن كَانُواْ صَـٰدِقِینَ ﴿٤١﴾

Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli.

Kwani wanao wanao shirikiana nao, na wanao fuata mwendo wao katika kauli yao hii? Basi na wawalete hao washirika wao, ikiwa wao ni wasema kweli katika madai yao.


Arabic explanations of the Qur’an:

یَوۡمَ یُكۡشَفُ عَن سَاقࣲ وَیُدۡعَوۡنَ إِلَى ٱلسُّجُودِ فَلَا یَسۡتَطِیعُونَ ﴿٤٢﴾

Siku utakapo wekwa wazi mundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza,

Siku mambo yatapo shitadi na yakawa magumu, na wakatakiwa makafiri wasujudu kwa kuwaemea na kuwakejeli, na wasiweze, (Kuwekwa wazi mundi, ni kinaya ya kudhihirishwa kweli yote Siku ya kwima kondo, Siku ya Kiyama. Chambilecho Sayyid Abdulla bin Ali bin Nassir katika Al Inkishaf: Tafakari siku ya kwima kondo Ya kuaridhiwa kila kitendo Pindi madhulumu atapo ondo Achamba Ya Rabi namua naye)


Arabic explanations of the Qur’an:

خَـٰشِعَةً أَبۡصَـٰرُهُمۡ تَرۡهَقُهُمۡ ذِلَّةࣱۖ وَقَدۡ كَانُواْ یُدۡعَوۡنَ إِلَى ٱلسُّجُودِ وَهُمۡ سَـٰلِمُونَ ﴿٤٣﴾

Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima

Macho yao yameinama chini, yamefunikwa na fedheha. Na duniani walikuwa wakitakiwa wasujudu walipo kuwa wakiweza na wakakataa kusujudu.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَذَرۡنِی وَمَن یُكَذِّبُ بِهَـٰذَا ٱلۡحَدِیثِۖ سَنَسۡتَدۡرِجُهُم مِّنۡ حَیۡثُ لَا یَعۡلَمُونَ ﴿٤٤﴾

Basi niache na wanao kadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua.

Ewe Muhammad! Nachilie na hao wanao ikadhibisha Qur'ani. Tutawajongeza kwenye adhabu kidogo kidogo kwa jiha wasio ijua kuwa adhabu itatokea huko.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَأُمۡلِی لَهُمۡۚ إِنَّ كَیۡدِی مَتِینٌ ﴿٤٥﴾

Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara.

Na nitawapa muhula kwa kuiakharisha adhabu. Hakika mipango yangu ni ya nguvu, na hawezi kuporonyoka yeyote akasalimika nayo.


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمۡ تَسۡـَٔلُهُمۡ أَجۡرࣰا فَهُم مِّن مَّغۡرَمࣲ مُّثۡقَلُونَ ﴿٤٦﴾

Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo?

Kwani wewe unawaomba ujira kwa kuufikisha Ujumbe wako, na kwa hivyo wao wanaona uzito kwa gharama hiyo unayo wakalifisha?


Arabic explanations of the Qur’an:

أَمۡ عِندَهُمُ ٱلۡغَیۡبُ فَهُمۡ یَكۡتُبُونَ ﴿٤٧﴾

Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika?

Au kwani wao wanajua yaliyo fichikana na wao wanayaandika na ndio wanahukumu kwa hayo?


Arabic explanations of the Qur’an:

فَٱصۡبِرۡ لِحُكۡمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُن كَصَاحِبِ ٱلۡحُوتِ إِذۡ نَادَىٰ وَهُوَ مَكۡظُومࣱ ﴿٤٨﴾

Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, alipo nadi naye kazongwa.

Basi wewe subiri kwa tunavyo wapa muhula na kukuakhirisha kukuletea manusura yetu juu yao. Wala usiwe kama Yunus, aliye mezwa na samaki, akawa na haraka na kuwaghadhibikia watu wake, alipo mnadia Mola wake Mlezi, naye kajaa hasira na ghadhabu, akitaka waadhibiwe kwa haraka.


Arabic explanations of the Qur’an:

لَّوۡلَاۤ أَن تَدَ ٰ⁠رَكَهُۥ نِعۡمَةࣱ مِّن رَّبِّهِۦ لَنُبِذَ بِٱلۡعَرَاۤءِ وَهُوَ مَذۡمُومࣱ ﴿٤٩﴾

Kama isingeli mfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa.

Lau kuwa neema ya Mola wake Mlezi haikumdiriki kwa kukubali toba yake, angeli tupwa kutokana na tumbo la samaki ufukweni, naye akiteseka kwa kuteleza kwake.


Arabic explanations of the Qur’an:

فَٱجۡتَبَـٰهُ رَبُّهُۥ فَجَعَلَهُۥ مِنَ ٱلصَّـٰلِحِینَ ﴿٥٠﴾

Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema.

Lakini Mola wake Mlezi kamteuwa kwa kuikubali toba yake, na akamjaalia miongoni mwa watu wema.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَإِن یَكَادُ ٱلَّذِینَ كَفَرُواْ لَیُزۡلِقُونَكَ بِأَبۡصَـٰرِهِمۡ لَمَّا سَمِعُواْ ٱلذِّكۡرَ وَیَقُولُونَ إِنَّهُۥ لَمَجۡنُونࣱ ﴿٥١﴾

Na walio kufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanapo sikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu.

Na makafiri wangeli karibia kukutelezesha na pahala pako, kwa jicho lao wanalo kuangalia kwa uadui na chuki wanapo isikia Qur'ani, wakisema: Hakika huyu ni mwendawazimu.


Arabic explanations of the Qur’an:

وَمَا هُوَ إِلَّا ذِكۡرࣱ لِّلۡعَـٰلَمِینَ ﴿٥٢﴾

Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

Na Qur'ani si chochote ila ni mawaidha, na hikima, na ukumbusho kwa walimwengu wote.


Arabic explanations of the Qur’an: